Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Kwa ufupi
Akizungumza na gazeti hili jana, Nape alisema:
“Mchakato wote wa Katiba Mpya unasimamiwa na sheria na sio maneno ya
Warioba. Sheria inazungumzia haki, wajibu na mamlaka ya Bunge hilo,
hivyo inawezekana kabisa kuboreshwa na hata kubadilishwa kwa hoja.”
Dar es Salaam. Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema
Bunge Maalumu la Katiba, litatekeleza majukumu yake kwa kufuata Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba na si mawazo ya mtu yeyote.
Kauli hiyo ya Nape imekuja siku moja baada ya
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kusema
kuwa litakuwa jambo lisilo la kawaida kwa Bunge hilo kubadili hoja ya
msingi iliyopo kwenye Rasimu ya Katiba, akisisitiza kuwa jukumu lake ni
kuifanyia marekebisho.
Warioba alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza
katika mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD),
kuhusu tafakuri na maridhiano kuelekea katika Katiba Mpya.
Alisema kama Bunge Maalumu la Katiba likipewa
jukumu la kuandika Katiba linaweza kubadili mambo mengi, lakini kama
Katiba itakuwa imeandaliwa na chombo kingine, Bunge hilo linatakiwa
kutobadili hoja za msingi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Nape alisema:
“Mchakato wote wa Katiba Mpya unasimamiwa na sheria na sio maneno ya
Warioba. Sheria inazungumzia haki, wajibu na mamlaka ya Bunge hilo,
hivyo inawezekana kabisa kuboreshwa na hata kubadilishwa kwa hoja.”
Nape alisema kulingana na sheria hiyo, Bunge hilo
lina mamlaka ya kufanya jambo lolote katika Rasimu hiyo, ikiwa ni pamoja
na kuifanyia maboresho kadri itakavyoonekana kuwa inafaa.
“Bunge haliwezi kutishwa na mtu yeyote kwa sababu
lipo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi. Ndiyo maana baada ya Bunge
hilo kwisha wananchi watapiga kura ya maoni,” alisema.
Akitolea ufafanuzi kauli ya Jaji Warioba kwamba
Bunge hilo lifanye maboresho na si kubadili hoja za msingi, Nape
alisema: “Maboresho maana yake ni kubadili. Ukiwa na nyumba ya vyumba
vinne na kuiboresha kwa kuweka chumba kimoja si umeibadili?”
Alisema Bunge hilo linatakiwa lisiingiliwe katika uamuzi wake.
0 comments:
Post a Comment