Tuesday, 18 February 2014

Utajiri wa Mbunge Vicky Kamata balaa….Ahususishwa na Freemason

vickykamata
WANAWAKE na maendeleo, tufanye kazi, tusonge mbele, yelele…yelele… Hii sehemu ya mashairi ya wimbo wa staa wa muziki wa kizazi kipya na Mbunge wa Viti Maalum (UVCCM), Geita, Vicky Kamata anayetajwa kuwa na utajiri balaa.

UWAZI LINA KILA KITU
Vicky amepata mafanikio makubwa ambayo kila mwanamke Tanzania angependa kuyapata. Gazeti hili lilimchimba kwa kina na kupata utajiri wote alionao kwa sasa.

KABLA YA SIASA, KABLA YA BONGO FLEVA
Kabla ya siasa aliishi maisha ya dhiki ambayo hakutegemea kama angekuja kupata mafanikio makubwa. Ni miongoni mwa Watanzania waliozaliwa katika familia duni.
Katika kutafuta ‘kutoka’ kimaisha, Vicky amewahi kuwa mwanamuziki wa Bongo Fleva na kutunga nyimbo mbalimbali, wimbo wa Wanawake na Maendeleo ndiyo uliomtambulisha zaidi katika jamii.

“Nimezaliwa kwenye familia duni, nimeishi maisha ya dhiki sana, mbali na muziki, nimewahi kuwa mwalimu wa shule ya msingi kule Moshi (Kilimanjaro) katika harakati za kusaka maisha, baadaye nilikwenda Morogoro.

“Kila kitu kinabadilika kama ukimwamini Mungu,” alisema Vicky mwenye watoto wawili, Revocatus na Glory (jina la baba halikutajwa).

MAFANIKIO YAANZA
Mwaka 2006, Vicky alifanikiwa kuajiriwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akiwa ni afisa uhusiano.
Mwaka 2010, Vicky alifanikiwa kuwa mbunge wa viti maalum akiuwakilisha Mkoa wa Geita.

MJENGO WA GHOROFA MBILI
Akiwa mbunge, Mheshimiwa Vicky ameingia kwenye orodha ya wanawake mabilionea nchini kwa kuangusha mjengo wa kifahari wa ghorofa mbili Sinza jijini Dar es Salaam wenye thamani ya shilingi bilioni moja na milioni mia nne.

Ndani ya ghorofa hilo kuna bwawa la kisasa la kuogelea ‘swimming pool’ ambalo linatumiwa na familia yake.
Mbunge wa Viti Maalum (UVCCM), Geita, Vicky Kamata.

MAGARI YAKE SASA
Kama walivyo matajiri wengine, mheshimiwa huyo anamiliki magari manne ya kifahari, yote yakiwa na thamani ya shilingi milioni 261.
Ana Toyota Voxy- Noah ambalo alilitoa sokoni kwa shilingi milioni 16.
Kamata pia anamiliki BMW X5 likiwa na thamani ya shilingi milioni 130.

Mara nyingi anapokwenda bungeni, Vicky hutembelea gari linalomudu mikiki ya barabarani, Toyota Land Cruiser ‘VX’ ambalo lina thamani ya shilingi milioni 90.
Pia mwanamama huyo ana gari aina ya Toyota Altezza alilolinunua kwa shilingi milioni 25.

ANAMILIKI MGODI WA DHAHABU
Wakati hayo yakiwa wazi, chanzo makini kilidai kuwa, mheshimiwa huyo amenunua mgodi wa dhahabu Geita, jambo ambalo ni sehemu kubwa ya mafanikio yake.

“Vicky amenunua mgodi wa dhahabu Geita, mimi ni mtu wangu  wa karibu, hapendi kusema mafanikio yake wala watu wajue lakini ukweli ndiyo huo. Eneo ni kubwa, muda si mrefu uchimbaji utaanza,” kilisema chanzo cha habari kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.

ANA SHAMBA LA EKARI 157
Utajiri wa mheshimiwa huyo unaendelea kuanikwa kuwa, ni pamoja na shamba  lenye ekari 150, Kisarawe, Mkoa wa Pwani. Pia ana shamba la miti Kibamba, Dar lenye ekari 7.

NI MFUGAJI
Mbali na mambo mengine, Vicky ni mfugaji kama ilivyo asili ya Wasukuma. Anafuga ndege aina ya kanga, kuku wa kisasa na mbuzi.

ANASOMESHA WATOTO WASIOJIWEZA
Katika mambo ambayo huenda yanachangia kuchota baraka, mheshimiwa Vicky anawalipia ada ya sekondari watoto yatima, walemavu na wasiojiweza kimaisha, idadi yao ikifikia 75.

KIPATO CHAKE KIKOJE?
Dodoso zinaonesha kwamba, kwa kazi ya uheshimiwa, kwa mwezi anaingiza shilingi milioni 15 ukijumlisha posho zote za ubunge, ujumbe wa kamati ya bunge na mshahara.

AMFUNIKA ANNE MAKINDA
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, jumba la kifahari la Vicky Kamata linalifunika lile la bosi wake ambaye ni spika wa bunge, mheshimiwa Anne Makinda. Yeye nyumba yake ipo Kijitonyama.

ULINZI NYUMBANI KWAKE USIPIME
Uwazi lilipata bahati ya kufika nyumbani kwa Vicky  na kukumbana na ulinzi wa mitambo ya kisasa ya kuzuia wezi na majambazi kwa saa 24.
Ili mgeni aingie ndani ya geti huhojiwa na walinzi kwa dakika zisizopungua kumi.

WABAYA WAKE WAMUUNDIA ZENGWE LA FREEMASON
Huwezi kupendwa na kila mtu, hii ni baada ya mwandishi wa gazeti hili kuamua kupiga kambi kwa muda wa siku mbili jirani na nyumba ya mheshimiwa huyo ambapo baadhi ya watu waliohojiwa kuhusu ukwasi wa mbunge huyo mwanamke walisema huenda ni memba wa Freemason.

“Mafanikio ya mbunge huyu bwana ni makubwa mno, tunasikia watu wakisema huenda ni Freemason. Lakini ndivyo tulivyo Watanzania, mtu akifanikiwa kidogo wanasema ni Freemason, ninavyomfahamu huyu dada amepiga hatua, sijawahi kumsikia na mambo ya Freemason,” alisema jirani mmoja na kuungwa mkono na wenzake.

MSIKILIZE VICKY
Katika mahojiano maalum na Uwazi kuhusu utajiri wake, Vicky alisema:
“Mafanikio yote yametokana na juhudi zangu za kujituma katika kufanya kazi, namwamini Mungu siku zote. Hakuna dhambi mbaya hapa duniani kama kukata tamaa.

“Tukifanya kazi kwa kujituma na kumwamini Mungu hakuna Mtanzania maskini.
“Kila mtu ana uwezo wa kubadilisha mfumo wa maisha akiamua, umaskini wa watu si chaguo la Mungu, kila jambo litokealo kwa mwanadamu lina maana kubwa kwa Mungu.”

KAULI YA UWAZI
Wanawake nchini waige mfano wa Vicky kwa kukamata fursa mbalimbali na wanapofanikiwa wawasaidie wengine, kama kusomesha yatima na wasiojiweza.

0 comments:

Post a Comment