HARAKATI za kuwania urais mwaka 2015 ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), zimefika hatua mbaya ya watu wanaotajwa kuwa katika orodha ya wagombea na wapambe wao kuingiwa na hofu ya kudhuriana na kuombeana mabaya,
Hofu hiyo imeongezeka zaidi hasa kutokana na ugonjwa wa ajabu anaougua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ambao taarifa zisizo rasmi zinauhusisha na kuwapo kwa mikono ya watu.
Ingawa hadi sasa si Mwakyembe mwenyewe au mamlaka yoyote ya umma aliyetoa taarifa rasmi ya nini hasa anaugua mwanasiasa huyo, lakini kauli ambazo alizitoa siku chache zilizopita zinaongeza chumvi katika mashaka hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mwakyembe aliyerejea kutoka katika matibabu nchini India alisema hana sababu ya kulipiza kisasi na kwamba anamwachia Mungu.
Kauli hiyo imeibua maneno mengi miongoni mwa wanasiasa ambao baadhi wamekuwa wakiitafsiri kuwa inayothibitisha wasiwasi uliotanda kwamba huenda mwanasiasa huyo anaugua kutokana na kudhuriwa na wanasiasa washindani wake.
Wakati ugonjwa anaougua Mwakyembe ukiwa bado unazusha mashaka, kuugua kwa muda mrefu kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Mark Mwandosya nako kuliibua maneno mengi.
Habari ambazo zilimkariri Mwandosya mwenyewe na watu walio karibu naye zinaeleza kwamba, ugonjwa wake ulisababisha baadhi ya wanasiasa ndani ya CCM kumchulia kifo kutokana na maradhi hayo.
Kabla na baada ya kurejea nchini kutoka katika matibabu yake nchini India, Mwandosya alikaririwa akisema watu waliokuwa wakimchulia kifo, walitakiwa kutambua kwamba watalazimika kusubiri kwa muda mrefu kabla ya hilo (kifo) kumfika.
Wakati hali ikiwa hivyo, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umebaini kuwa, kumekuwa na hali ya kutoaminiana na kutiliana sana mashaka miongoni mwa makada maarufu ndani ya CCM ambayo yote inahusishwa na mchakato wa urais ndani ya chama hicho mwaka 2015.
Kada mmoja maarufu wa CCM aliyezungumza na Tanzania Daima Jumatano amesema wamefikia hatua ya kujilinda kwa kuwa waangalifu katika matembezi na sehemu wanazokula chakula kwa sababu hizo hizo.
Kwa mujibu wa kada huyo, wanasiasa takriban wote wanaotajwa kuwa wanatarajia kugombea urais kupitia chama hicho wamefikia hatua ya kujilinda kwa silaha za moto na wengine kutumia mafuta maalum yanayoaminika kuzuia sumu.
“Tumefika pabaya, hali ni ngumu sana. Sasa hivi watu wamegawana hata maeneo ya kutembelea. Kwa mfano kama kundi fulani lina kawaida ya kupata bia kwenye baa au hoteli fulani, makada wa kundi lingine hawafiki.
“Ikitokea mmekutana kwa bahati mbaya, mmoja lazima aondoke,” alisema mmoja wa makada wanaotajwa kuwania urais.
Kiongozi mmoja mstaafu anayetajwa kuwa miongoni mwa wagombea urais naye anaelezwa kwamba amelazimika kuchukua hatua kadha wa kadha za kujilinda ili kuepukana na hatari ya kudhuriwa na washindani wake wa kisiasa ndani ya CCM.
“Hivi sasa tumefika mahali tunasafiri kwa tahadhari kubwa na kwa kutumia usafiri ambao baadhi ya watu wanaotulenga hawawezi kututambua kama njia ya kukabiliana na hatari ambayo inahusishwa na urais wa mwaka 2015,” amekaririwa akisema mwanasiasa huyo mstaafu.
Wakati hayo yakitokea kumbukumbu zinaonyesha kwamba kwa nyakati tofauti wanasiasa wawili, akiwamo Mwakyembe mwenyewe na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta wamepata kutoa taarifa za maisha yao kutishiwa.
Sitta ambaye duru za kisiasa zinamtaja kuwa mmoja wa wanaofikiria urais, amepata kukaririwa kwamba amekuwa akipokea vitisho vya kuuawa kupitia simu yake ya mkononi kwa njia ya ujumbe mfupi na watu asiowajua.
Mgombea mwingine ambaye jina lake nalo limehusishwa na tishio la maisha yake ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Gazeti moja la kila wiki (siyo Tanzania Daima) lilipata kumkariri mtoto wa mwanasiasa huyo akilalamika kuhusu kuwapo kwa tishio la maisha ya mzazi wake huyo.
Ingawa wenyewe hawajatamka rasmi, baadhi ya makada wengine wanaotajwa kufukuzana kurithi nafasi ya Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015 ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Dk. Emmanuel Nchimbi, Hussein Mwinyi na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda.
Majina ya wanasiasa wengine wanaotajwa ni pamoja na Mathias Chikawe, John Magufuli, William Ngeleja, Lazaro Nyalandu na Ezekiel Maige.
Katika hatua nyingine, wakati Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), unatarajiwa kufanyika mwaka huu, chama hicho kimejikuta kikiingia kwenye vita mpya ya kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wazee na ile ya Umoja wa Vijana (UVCCM).
Ugumu wa uchaguzi huo, unatokana na makundi yanayowania urais ndani ya CCM mwaka 2015 kufanya kila iwezalo kuhakikisha inamwingiza mtu wake ambaye atapata nafasi ya kuingia kwenye vikao muhimu vya maamuzi, yaani Halmashauri Kuu (NEC) na Kamati Kuu (CC).
Tayari makundi hayo ya urais yameshaanza harakati za kuhakikisha yanashika nafasi hizo nyeti kwa gharama yoyote ile.
Kiti cha Mwenyekiti wa Wazazi CCM, kimeachwa wazi baada ya aliyekuwa kiongozi wa nafasi hiyo kufariki wiki iliyopita wakati nafasi ya umoja wa vijana iko wazi baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Masauni Masauni, kuamua kujiuzulu kutokana na kashfa ya kughushi umri wake.
0 comments:
Post a Comment