JEURI
ya wazi inayoonekana kuwemo ndani ya taarifa ambazo zimekuwa
zikichapishwa mara kwa mara na vyombo vya habari vya serikali ya Rais
Paul Kagame wa Rwanda dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na serikali yake,
inaelezwa kujengwa na ushirika wake wa kiintelijensia alioupandikiza
ndani ya mfumo wa serikali na taasisi mbalimbali hapa nchini,MTANZANIA
limedokezwa. Taarifa
zilizolifikia gazeti la MTANZANIA kutoka kwa watu waliokaribu na
viongozi wa Rwanda na wale walioko kwenye taasisi mbalimbali za
kiserikali hapa nchini,zinaeleza kuwa taarifa ambazo zimekuwa
zikiripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo, msingi wake
unaweza kuwa mtandao ambao serikali ya Kagame imeujenga hapa nchini.
Kwamba
Rwanda, mbali na kufanikiwa kupenyeza watu wake kwenye mifumo ya
kitaasisi hapa nchini, pia imefanikiwa kujenga ushirika na watu wa kada
mbalimbali wenye umaarufu,ushawishi na wanaoheshimika nchini, wakiwemo
baadhi ya wasomi na wanasiasa.
Kuvuja kwa taarifa hizi, kumekuja wakati ambao gazeti la serikali ya Rwanda,Rwanda Times na mtandao wa News of Rwanda, yakiripoti taarifa zinazoigusa serikali ya Rais Kikwete, ikinukuu vyanzo vya kutoka hapa nchini, japo ukweli wa taarifa hizo ukiwa haujulikani,kutokana na Ikulu ya Dar-es-salaam kuzikanusha mara kwa mara.
Dhana hii inapewa nguvu na taarifa mpya kabisa zilizotufikia, ambazo zinadai kuwa katika kuendelea kuimarisha mtandao wake, Serikali ya Rwanda imechangisha fedha kwaajili ya baadhi ya vyama vya siasa hapa nchini ili kulinda maslahi yake.Taarifa hizo zinamtaja Waziri wa Miundombinu wa nchi hiyo, Profesa Silas Lwakabamba, ambae aliwahi kusoma na kuishi nchini kuwa ndiye aliye endesha harambee hiyo ambayo inadaiwa ilimshirikisha Rais Kagame. Habari zaidi ambazo MTANZANIA imezipata zinadai kuwa katika harambee hiyo, iliyohudhuriwa na baadhi ya Mawaziri wa serikali ya Rwanda pamoja na wafanyabiashara wakubwa nchini humo,Rais Kagame kwa upande wake alichangia Dola 500,000.
Gazeti hili limedokezwa kuwa, lengo la harambee hiyo, ni kuhakikisha ushawishi wake unafanikiwa, hasa kwa watu ambao wamekuwa wakiiunga mkono Rwanda, hususani wakati huu mgumu ambao inakabiliwa na tuhuma za kuchochea mapigano katika eneo la Mashariki ya Congo, ambako Tanzania imepeleka wanajeshi wake.
Katika mkakati huo, walengwa ni vyama vya upinzani, kutokana na kuwa na uhusiano wa shaka na serikali iliyoko madarakani.
Tayari mara kadhaa vyombo vya habari Rwanda, hususani vile vya serikali, vimekuwa vikitumia kauli zinazotolewa na wapinzani hapa nchini, kama hoja ya utetezi wake dhidi ya uhusiano mbaya na Ikulu ya Dar-es-salaam.
Profesa Lwakabamba, ambaye anatajwa kuongoza zoezi la sasa, inaelezwa kuwa serikali ya Rwanda imeamua kumtumia kutokana na uelewa wake kuhusu Tanzania.
Kabla ya taarifa hizi, Lwakabamba aliwahi kuripotiwa na gazeti moja (si MTANZANIA) kwamba ni waziri mwenye asili ya Tanzania aliyechaguliwa katika serikali ya Rwanda.
Inaelezwa kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, lakini pia alisoma Chuo Kikuu Dar-es-salaam (UDSM) Kitivo cha Uhandisi, na mwaka 1981 alikuwa Mkuu wa kitivo cha Uhandisi, kazi aliyoifanya mpaka anaondoka nchini.
Profesa Lwakabamba, ambaye anaelezwa kuijua vyema Tanzania kutokana na kuishi muda mrefu, alipata elimu ya msingi Muleba, mkoani Kagera na baadaye kujiunga na shule ya sekondari ya Ihungo.
Mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu katika Kitivo cha Uhandisi, baada ya kujiunga na Chuo cha Leeds, Uingereza kwaajili ya shahada ya fani hiyohiyo.
Msomi huyo anaelezwa kwenda Rwanda mwaka 1997,baada ya kuombwa na Rais Kagame, ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu katika taifa lake, baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.
Gazeti hili lilimtafuta Profesa Lwakabamba kwa njia ya mtandao ili kupata ufafanuzi kuhusiana na harambee hiyo, lakini hakuweza kujibu maswali aliyoulizwa.
Juhudi za kumtafuta Profesa Lwakabamba bado zinaendelea. Wakati hayo yakitokea,taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa katika mkakati huo,mbunge mmoja (jina tunalo), hivi karibuni alisafiri kwenda Rwanda akipitia Afrika Kusini.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo alionana na baadhi ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Rais Kagame kuhakikisha anaimarisha mtandao wake hapa nchini.
Mbali na mbunge huyo,taarifa hizo zimewataja baadhi ya wanasiasa wengine ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakifaidika na fedha za serikali ya Rais Kagame, kwa kujua ama pasipo kujua kama lengo lake ni kuwaweka katika mtandao wake huo.
0 comments:
Post a Comment