MKAZI wa Korogwe, mkoani Tanga ambaye inadaiwa alilazwa katika Hospitali ya Wagonjwa wa Akili Lutindi, wilayani humo,
hivi karibuni alitoa kali ya mwaka baada ya kutoka wodini, kuingia katika gari ambalo dereva wake alikuwa hajalizima na kuondoka nalo akiendesha mwenyewe.
Tukio hilo lilivuta hisia za watu wengi waishio jirani na hospitali hiyo, ambapo dereva wa gari hilo alifahamika kwa jina moja la Bw. Wikama ambaye aliliacha gari hilo likiwa halijazimwa.
Akizungumza na gazeti hili, Diwani wa Viti Maalumu Tarafa ya Bungu, Bi. Elizabeth Singano, alisema mgonjwa huyo wa akili ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, aliendesha
gari hilo na kushuka nalo katika milima yenye miteremko mikali
yenye kona bila wasiwasi wowote.
“Ilibidi zipigwe simu ili kuomba msaaada wa kulizuia gari ndipo wananchi waliamua kuweka magogo barabarani ili kulizuia,” alisema Bi. Singano anayekaa kitongoji cha Bethelehemu
kilichopo jirani na hospitali hiyo.
Aliongeza kuwa, Bw. Wikama alifika katika kituo hicho baada ya kupeleka mgonjwa wa akili na alipoteremka kwenye gari hakulizima ndipo mgonjwa huyo aliingia na kulichukua.
“Watu walishtuka walipoona mgonjwa wa akili akiendesha gari, walianza kupiga kelele wakati akiondoka nalo lakini mwenyewe hakuonesha waziwasi wowote,” alisema.
Majira lilipomtafuta Bw. Wikama ambaye ni mkazi wa Donge, jijini humo kwa njia ya simu ili kuzungumzia mkasa huo, alikiri kutokea tukio hilo na kudai kuwa, asingependa kulizungumzia kwa kina kwani gari hilo ni mali ya ofisi si la kwake.
“Ni kweli bwana mgonjwa wa akili aliendesha gari nililokwenda nalo hospitali ila nisingependa kulizungumzia sana tukio hilo, wapo watakaolipokea tofautina,” alisema Bw. Wikama ambaye alipotakiwa kutaja namba za gari na aina yake alikata simu
na alipopigiwa tena hakupokea.
Hata hivyo, Ofisa Utawala wa hospitali hiyo aliyefahamika kwa jina moja na Bw. Lauth, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai mgonjwa huyo wamemrudisha Dar es Salaam.
Alisema tukio hilo halikuwa la kawaida lakini limetokea kwa sababu aliyefika na gari hospitalini hapo hakulizima kama ilivyo kawaida ya madereva wanaopeleka wagonjwa ili kuepuka matukio ya aina hiyo.
0 comments:
Post a Comment