Saturday, 15 February 2014

Maajabu ya ‘Shimo la Mungu’ Newala

 

Mkazi wa Newala, Maimuna Pinda  akionyesha eneo la ‘Shimo la Mungu’, sehemu ambayo pia wenyeji wa wilaya hiyo hufanyia matambiko.
Kwa ufupi
  • Asili yake ni kitendawili, yadaiwa ndege haziwezi kuruka juu yake

Newala. Katika Wilaya ya Newala, mkoani Mtwara lipo shimo la ajabu lijulikanalo kama ‘Shimo la Mungu’ lililochukua robo tatu ya ukubwa wa wilaya hiyo.
Shimo hili linalotajwa kuwa moja ya vivutio mkoani Mtwara limesheheni hifadhi za misitu, mito, mabonde, mawe ambayo yanapendeza kwa macho pia kipo kisima cha maji Newala.
Jambo hili linawasumbua wale wanaojua historia yake ni taarifa za kutupwa kwa watoto, kupotea kwa watu wale wanaojaribu kuingia bila ruhusu, wabishi wasioamini tambiko na mambo mengine kadhaa ambayo hata hivyo ni vigumu kuyathibitisha.
Ni shimo la asili ambalo limekuwapo miaka mingi, na wenyeji wa Mji wa Newala wanaliita ‘Shimo la Mungu’ kutokana na kile wanachoeleza kuwa ni maajabu ambayo hutokea yakianzia katika shimo hilo.
Miongoni mwa maajabu hayo ni yale ambayo hutokea nyakati za asubuhi kipindi cha masika ambapo upepo mkali sana huvuma kutoka lilipo shimo hilo.
Wanasema wakati mwingine hutokea moshi mzito ambao husambaa na kuufunika Mji wa Newala na kusababisha giza nene katika makazi ya watu kiasi cha watu kushindwa kuonana kwa kati ya dakika tatu na dakika saba.
Mkazi wa Newala, Sophia Saidi (90) anasema: “Sisi tumezaliwa tumelikuta, kutokana na shimo hilo kutotengenezwa na mtu yeyote ndio maana tukaliita ‘Shimo la Mungu”.
Bibi Sophia kama anavyojulikana na wengine anasema anaongeza: “Sehemu hiyo huwa panatokea miujiza kama hiyo ambayo inaleta upepo mkali, mara giza hata sisi hatujuwi ni nani ambaye ana sababisha kuwe na giza kutoka sehemu ya shimo hilo hadi sehemu ya makazi ya watu”.
Kutokana na umaarufu wake, eneo hilo limekuwa kivutio kikubwa cha watu ambao hufika kwa ajili ya kufanya matambiko ya jadi, ikiwa ni sehemu ya mila na desturi za wakazi wa Newala na wilaya nyingine jirani.
Maimuna Pinda (55) ambaye pia ni mwenyeji wa eneo hilo anasema hata waganga wa jadi kuingia na kutoka ndani ya ‘Shimo la Mungu’ kwa ajili ya kuchukua dawa mbalimbali za miti shamba ambazo hutumika kutibia magonjwa kadhaa. Pinda anasema kabla ya mtu hajaingia ndani ya shimo hilo ili kutalii au kuchukua dawa, lazima afanywe tambiko.
Pembezoni mwa shimo hilo huota uyoga ambao ni kitoweo kwa wakazi wanaolizunguka, lakini kwa maelezo ya wenyeji uchumaji huo huwa ni hatari kwani mara kadhaa watu wamepoteza maisha kutokana na kupatwa na kizunguzungu kisha kutumbukia kwenye shimo.

0 comments:

Post a Comment