Sumbawanga. Mwanamke mmoja mkazi wa Kijiji cha Mnyamasi, Wilaya ya
Mpanda mkoani Katavi, Tatu Mihambo (20) amejeruhiwa vibaya baada ya
kupigwa na mumewe kwa fimbo na kisha kumwagiwa maji ya moto kwa madai ya
kukasirishwa na kitendo cha kumuomba fedha ya matumizi.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba, tukio hilo la ukatili wa
kijinsia lilitokea juzi, saa 7 mchana, nyumbani kwa wanandoa hao kijiini
hapo ambapo inadaiwa kuwa mwanamke huyo ni mke wa pili wa Juma Masasila
aliyefanya kitendo hicho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema siku
ya tukio, Tatu alimtaarifu mumewe kuwa anajisikia kuumwa na kichwa
hivyo alimuomba fedha ili akatafute dawa ya kupunguza maumivu.
Alisema kitendo hicho kilimkera mumewe na ndipo alipomueleza mkewe
kuwa, ukoo wao huwa hawatumii dawa zinazouzwa kwenye maduka ya dawa na
kumtaka akatafute dawa za miti shamba sambamba na kwenda haraka shambani
kufukuza Tumbili wasile mazao.
Kidavashari alieleza kuwa Tatu alitii agizo hilo la mumewe la kwenda shamba kulinda mazao huku kichwa kikiendelea kumuuma.
Alieleza ilipofika saa 12.00 jioni, Tatu alirejea nyumbani huku akiwa
na maumivu makali ya kichwa na alimsisitiza mume wake aende dukani
kumnunulia dawa.
Badala ya mumewe kwenda kumtafutia dawa dukani alianza kumshutumu mkewe kuhusu upotevu wa panga.
Mkewe alikataa madai hayo na majibu hayo yalimkera mtuhumiwa
aliyeanza kumshambulia mkewe kwa fimbo na kisha alichukua maji ya moto
na kumumwagia mkononi na kwenye makalio .
Inaelezwa kuwa Tatu aliendelea kuugulia maumivu yake akiwa nyumbani
bila kupata matibabu yoyote na vidonda kuanza kutoa harufu ndipo mume
aliposhtuka na kumpeleka kijiji cha jirani cha Lwafi kwa ajili ya
matibabu ya dawa za kienyeji.
Inasemekana walipofika kijijini hapo watu walishtushwa na hali ya
mgonjwa huyo na kumuhoji mtuhumiwa aliyewadanganya kuwa alianguka kwenye
mti wa ukwaju, lakini mkewe aliwaeleza ukweli na ndipo walipoanza
kumshambulia.
Kamanda Kidavashari alisema, baada ya muda taarifa ziliwafikia polisi
na walifika katika eneo hilo na kumkamata mtuhumiwa huyo na walimchukua
Tatu na kumkimbiza katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ambako amelazwa
akiwa anaendelea na matibabu huku hali yake ikiwa mbaya na anaongea kwa
tabu.
0 comments:
Post a Comment