Na
Mwandishi Wetu
Mchungaji Ambilikile Mwaisapila
(Babu wa Kikombe) wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amesema
Mungu ameendelea kujifunua kwake na kumuonesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha
Afrika na dunia kwa ujumla.
Alitoa kauli
hiyo juzi mbele ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa
kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri
Mkuu uliposimama nyumbani kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini
Arusha.
Mchungaji
Mstaafu Mwaisapila alisema kuna mambo mengi ambayo yameandikwa kwenye Biblia,
lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge.
“Mungu
ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi ni mzee
na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema huku
akishangiliwa na wananchi.
Alisema katika
mafunuo aliyopewa na Mungu ameoneshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika
kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa kugawa kikombe ikiwemo mahema, maji na
ulinzi.
Waziri Mkuu,
Pinda ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo na
migogoro ya ardhi yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa
za Ngorongoro, Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch.
Mwaisapila kwani Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo
vitabadili sura ya Taifa hili.
"Mungu
ametupa gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali.
Tuna makaa ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati
ya umeme kutoka ardhini (Geo-thermal) katika Ziwa Natron," alisema.
Alisema
Tanzania imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu
uliopo nchini. Aliwaeleza wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa
barabara atakuwa katika eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo
awamu ya kwanza itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi maalum kwa niaba ya vijana
mbele ya Waziri Mkuu, Elias Kalumbwa, alisema wanaomba kuchimbiwa bwawa ili
waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mboga na matunda.Kalumbwa ambaye amesomea masuala ya
wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo katika mto wa msimu unaopita
kijijini hapo.
Naye MarthaSereri (70) alimweleza
Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro ligawanywe kwa sababu ni kubwa
sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao kufika maeneo yote. Aliomba pia
wapatiwe walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo
kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe mikopo ya matreka ili
waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo ya matrekta na plau,
haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya. Ukikodisha trekta kila
ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi? Mkitukopesha matrekta mtakuwa
mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja hizo, Waziri Mkuu alisema
hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana kupatiwa bwawa ni jambo
linalowezekana kupitia mipango ya maendeleo ya kilimo ya wilaya (DADPS).
"Andaeni andiko lenu, inabidi
litoke kwa wananchi na si Serikalini. Mkituletea ni jambo linalowezekana kwani
liko ndani ya mipango ya wilaya," alisema.
Akijibu hoja kuhusu ukubwa wa jimbo,
Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana kuongeza jimbo isiwe
suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo lao.
"Kuongeza jimbo inaweza isiwe jibu
la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na jiografia ya eneo lenu,
kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale.
Mimi
nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa
wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka
kwenu," alisema.
0 comments:
Post a Comment