Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Dk Hamisi Kigwangalla amesema ili kuondoa mvutano kuhusu muundo
wa Muungano ni lazima yafanyike mambo mawili, ambayo ni kuongeza muda wa
Rais kuwa madarakani au kubadili Katiba katika maeneo yanayohusu Tume
ya Uchaguzi (NEC) pekee.
Akizungumza jijini jana, Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega
(CCM) alisema mambo hayo mawili hayawezi kukwepeka kwasababu hata kama
Katiba Mpya itapatikana, bado itahitajika kufanya mabadiliko ya sheria
mbalimbali, zoezi ambalo alidai litachukua takriban miaka miwili.
“Namwomba Rais Jakaya Kikwete aingilie kati. Atumie mamlaka yake
kusitisha mchakato wa Katiba mpaka itakapoundwa Tume nyingine ya
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la muundo wa Muungano,” alisema
na kuongeza;
“Baada ya maoni hayo ipigwe kura maalumu kuhusu jambo hili ili Watanzania washiriki kikamilifu na upatikane uamuzi sahihi na unaokubalika na wengi. Si jambo la busara kujadili Rasimu ya Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu muundo wa Muungano.”
Alisema kuwa kitendo cha Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na
Jaji Joseph Warioba kupendekeza muundo wa Serikali tatu, utalivuruga
Bunge la Katiba iwapo wataibuka wajumbe na kupinga muundo huo.
Alisema kuwa kama muundo wa Serikali tatu utapingwa, muundo wowote
utakaopitishwa utasababisha kuwekwa vifungu vipya jambo ambalo litazidi
kuleta mkanganyiko katika mchakato mzima wa Katiba.
“Ndiyo maana nikasema mchakato huu usitishwe kwa muda ili watu wote
tukubaliane juu ya muundo wa muungano tunaoutaka. Wabunge wa Bunge la
Katiba tukiukataa huu muundo wa Serikali tatu kipi kitatokea?”alihoji.
Dk Kigwangalla alisema Tume hiyo bado haijatoa majibu katika mambo
kadhaa; njia ilizotumia kupendekeza Serikali tatu, kwa nini
walipendekeza mfumo huo na nani atakuwa na mamlaka ya kuandika Katiba ya
Tanganyika.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati tayari Rais Kikwete ameshateua
wajumbe 201 wa Bunge hilo ambalo linaanza Februari 18 mjini Dodoma.
0 comments:
Post a Comment