Showing posts with label sisa. Show all posts
Showing posts with label sisa. Show all posts

Tuesday, 18 February 2014

Kagame adaiwa kupandikiza Makachero Nchini Kuipeleleza Serikali….Mbunge Atajwa kuhusika..!

kagame
JEURI ya wazi inayoonekana kuwemo ndani ya taarifa ambazo zimekuwa zikichapishwa mara kwa mara na vyombo vya habari  vya  serikali ya Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na serikali yake, inaelezwa kujengwa na ushirika wake wa kiintelijensia  alioupandikiza ndani ya mfumo wa  serikali  na taasisi mbalimbali hapa nchini,MTANZANIA limedokezwa. Taarifa zilizolifikia gazeti la  MTANZANIA  kutoka kwa  watu waliokaribu na viongozi wa Rwanda na wale walioko kwenye taasisi mbalimbali za kiserikali hapa nchini,zinaeleza kuwa taarifa ambazo zimekuwa zikiripotiwa na vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo, msingi wake unaweza kuwa  mtandao ambao serikali ya Kagame imeujenga hapa nchini. Kwamba Rwanda, mbali na kufanikiwa kupenyeza watu wake kwenye mifumo  ya kitaasisi hapa nchini, pia imefanikiwa kujenga ushirika na watu wa kada mbalimbali wenye umaarufu,ushawishi na wanaoheshimika nchini, wakiwemo baadhi ya wasomi na wanasiasa.
 paul
Kuvuja kwa taarifa hizi, kumekuja wakati ambao  gazeti la serikali ya Rwanda,Rwanda Times na mtandao wa News of Rwanda, yakiripoti taarifa zinazoigusa  serikali ya Rais Kikwete, ikinukuu vyanzo vya kutoka hapa nchini, japo ukweli wa taarifa hizo ukiwa haujulikani,kutokana na Ikulu ya Dar-es-salaam kuzikanusha mara kwa mara.
                                                                          
Dhana  hii inapewa nguvu na taarifa mpya kabisa  zilizotufikia, ambazo zinadai kuwa katika kuendelea kuimarisha mtandao  wake,  Serikali ya Rwanda  imechangisha  fedha  kwaajili  ya  baadhi ya vyama vya  siasa hapa nchini ili kulinda maslahi yake.Taarifa hizo  zinamtaja  Waziri wa Miundombinu  wa  nchi hiyo,  Profesa Silas Lwakabamba, ambae  aliwahi kusoma na kuishi nchini  kuwa ndiye aliye endesha  harambee hiyo  ambayo inadaiwa ilimshirikisha Rais Kagame. Habari  zaidi ambazo MTANZANIA  imezipata zinadai kuwa katika harambee hiyo, iliyohudhuriwa  na baadhi  ya  Mawaziri wa serikali ya Rwanda  pamoja na wafanyabiashara wakubwa nchini humo,Rais Kagame kwa upande wake alichangia  Dola 500,000.
Gazeti hili limedokezwa kuwa, lengo la harambee hiyo, ni kuhakikisha ushawishi wake unafanikiwa, hasa kwa watu  ambao wamekuwa wakiiunga mkono Rwanda, hususani wakati huu mgumu ambao  inakabiliwa na tuhuma za kuchochea mapigano katika eneo la Mashariki ya Congo, ambako Tanzania imepeleka  wanajeshi wake.
Katika mkakati huo,  walengwa ni vyama  vya upinzani, kutokana  na kuwa na uhusiano  wa shaka na  serikali iliyoko madarakani.
Tayari mara kadhaa  vyombo vya  habari  Rwanda, hususani vile vya serikali, vimekuwa vikitumia  kauli zinazotolewa na wapinzani  hapa nchini, kama hoja ya utetezi wake dhidi ya uhusiano mbaya na Ikulu ya  Dar-es-salaam.
Profesa Lwakabamba, ambaye anatajwa kuongoza zoezi la sasa, inaelezwa kuwa serikali ya Rwanda imeamua kumtumia kutokana na uelewa wake kuhusu Tanzania.
Kabla ya taarifa hizi, Lwakabamba aliwahi kuripotiwa na gazeti moja (si MTANZANIA)  kwamba ni waziri mwenye asili ya Tanzania aliyechaguliwa katika serikali ya Rwanda.
Inaelezwa kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda, lakini pia alisoma  Chuo Kikuu Dar-es-salaam (UDSM)  Kitivo cha Uhandisi, na mwaka 1981 alikuwa Mkuu wa kitivo cha Uhandisi, kazi aliyoifanya mpaka anaondoka nchini.
Profesa Lwakabamba, ambaye anaelezwa kuijua vyema Tanzania kutokana na kuishi muda mrefu, alipata elimu ya msingi Muleba, mkoani Kagera na baadaye  kujiunga na shule ya sekondari ya Ihungo.
Mwaka 1971 na 1975 alipata Shahada ya Uzamivu  katika Kitivo cha Uhandisi, baada ya kujiunga na Chuo cha Leeds, Uingereza kwaajili ya shahada ya fani hiyohiyo.
Msomi  huyo anaelezwa kwenda Rwanda mwaka 1997,baada ya kuombwa na Rais Kagame, ambaye alikwenda UDSM kuwaomba baadhi ya wahadhiri kwenda Kigali kufungua chuo kikuu  katika taifa lake, baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1994.
Gazeti hili lilimtafuta Profesa Lwakabamba kwa njia ya mtandao ili kupata ufafanuzi  kuhusiana na harambee hiyo, lakini hakuweza kujibu maswali aliyoulizwa.
 Juhudi za kumtafuta Profesa Lwakabamba bado zinaendelea. Wakati hayo yakitokea,taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa katika mkakati huo,mbunge mmoja (jina tunalo), hivi karibuni  alisafiri kwenda Rwanda  akipitia Afrika Kusini.
Inaelezwa kuwa mbunge huyo alionana na  baadhi ya viongozi wa serikali ya nchi hiyo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Rais Kagame kuhakikisha anaimarisha mtandao wake hapa nchini.
Mbali na mbunge huyo,taarifa hizo zimewataja baadhi ya wanasiasa  wengine ambao kwa muda mrefu  wamekuwa wakifaidika na fedha za serikali ya Rais Kagame, kwa kujua ama pasipo kujua  kama lengo lake ni kuwaweka katika mtandao wake huo.

Monday, 17 February 2014

“NI MARUFUKU KUTUMIA PESA KUNUNUA MADARAKA YA UONGOZI”…SOMA KUJUA,,,,,,,,,,

membe
WAZIRI  wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe
,amesema kuwa ni mwiko kwa mtu yeyote ndani ya chama kutumia fedha
kama nguzo ya ushindi wake kwa kuwa uongozi wa taifa hauwezi
kununuliwa na fedha.
Membe ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi(NEC) Mbali na hilo pia amekitaka chama hicho kufika mahala kuchagua ni nani anayefaa kuwa kiongozi kwa kufanya midahalo ili kutambulika kwa wananchi na kuepuka chama kumegukameguka.
membe
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
mara baada ya kutoka kuhojiwa na kamati ndogo ya maadili ya chama
hicho ambayo ilikaa tangu alhamis ya wiki iliyopita kwaajili ya
kuwahoji makada sita ambao wamejitangaza kuwania urais katika uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015 kinyume na sheria na taratibu.
Membe alitinga katika viwanja vya Makao Makuu ya CCM majira ya saa
tatu asubuhi na kutoka saa 4:54 asubuhi.
Alisema kuwa haiwezekani kuwa na kiongozi anayenunua uongozi kwa njia
yeyote ile, iwe ya fedha au jambo lolote na hilo ndilo kamati ya
maadili inakemea na yeye anaungana nayo.
“Lakini waandishi habari lazima wawe objective, waandishi lazima
mmpime, , waandishi wa habari ndio mnaoweza kuamua direction iende
wapi, lazima muandike ya watu wote wanayozungumza bila kuchagua mambo
Fulani ya mtu Fulani,”.
“Nawaambia waandishi chezeni mtaona, hatuwezi kuruhusu uongozi wa nchi
hii  au kiongozi wa juu anunuliwe kama biashara ya njugu dukani,
tukiacha hilo liendelee ninyi waandishi wa habari ni sehemu ya watu wa
kulaumiwa duniani,”alisema Membe
Alisema taifa la Tanzania litakuwa ni la ajabu kama watanzania
wataruhusu kufanya kufanya biashara ya uongozi wa kitaifa.
Hata hivyo alisema kuwa ni vyema sasa chama kikajipanga kuwa na
Mgombea ambaye wanachama wajue ni nani atakayepeperusha Bendera katika
uchaguzi wa Mwakani.
“Kwa mfano ili wananchi wajue tupokwenda mwaka 2015 candidate wa chama
ni nani, lazima tufike hapo tukiacha kila mwanachama aombe kila
binadamu anayeona anaavaa nguo ya kijani au ana hela aombe,
tutakiangusha chama chetu…Nadhani tunashauri chama kikajipange na
kiwe na candidates yaani kiwe na watu ambao  inabidi harakahara
wapitishwe ili CCM kinapofika desemba kwa mfano tuwe tunajua nani
anachukua bendera ya chama ili kisimegukemeguke,”alisema Membe
Aidha alisema kuwa alishauri kuwepo na muongozo rasmi unaotakiwa
kufuatwa na wanaccm kuanzia katika ngazi za matawi mpaka juu.
“Wakati wa uongozi utumie hatua zipo ili uzingatie nini ili usivunje
maadili, mashabiki nao wafanye nini ili wasikiuke maadili ili tuweze
kwenda pamoja kwa hiyo ni kamati ya maadili inayouliza maswali magumu
sana kwa watu wanaosemwa kwamba  wanaweza kuwa viongozi,”alisema Membe
Alisema kuwa kamati ya maadili inataka chama hicho mwakani kiende
katika uchaguzi kiwe imara na kuungana ili kuhakika wa ushindi na CCM
iendelee kupeta miaka 60 ijayo hakuna atakayeingia.
“Mimi ni miongoni mwa watu tulioitwa na kamati ya maadili, kamati
imefanya kazi nzuri, imedhamilia kumuita kila mtu anayetajwa kuwa
anaweza kuwa kiongozi,”alisema Waziri huyo.
Hata hivyo alisema kuwa kamati ya maadili imejipanga vizuru sana na
wasidanganyike.
“Wanauliza maswali magumu ama unayoyafanya wewe au wanayoyafanya
mashabiki lakini yote yanalenga chama chetu, kuimarisha ushindi 2015
na katika kuimarisha maadili,”alisema Waziri huyo
Hata hivyo alisema kuwa kumekuwepo na uzukaji ghafla wa
makundi makubwa ambayo yamezaliwa na kila watu wanadhani fulani
anafaa kuwa kiongozi.
“Tutafaanyaje nini ili chama kiwe na kundi moja litakalokwenda mwakani
kwenye ushindi na suala la fedha kama msingi wa ushindi, inatokeaje
watu wanatumia mamilioni mabilioni ya pesa katika kujinufaisha na
kujiandaa
kwenda kwenye uchaguzi,”aliema Membe
Aliitaka kamati ya maadili iendelee kuifanya  kazi hiyo na kudai kuwa
bado kuna wengine wataitwa lengo ni kuwa na chama imara ambacho
kitakwenda kwenye uchaguzi mwakani kwenda kuvishinda vyama vingine
vinavyojitokeza na vingine ambavyo vimeshaanza kufa.

HII NDIYO POSHO YA BUNGE LA KATIBA WANAYO PEWA KWA SIKU TSH 300, 000


 
BUNGE Maalumu la Katiba litafunguliwa rasmi Jumatano ijayo ya Februari 26, mwaka huu likiwa na wajumbe 629 na imethibitishwa kuwa kila mjumbe atalipwa Sh 300,000 kwa siku. Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Thomas Kashillilah, aliwaambia waandishi wa habari hayo jana ndani ya ukumbi mpya wa Bunge, walipoingia kwa mara ya kwanza ndani ya ukumbi huo kuangalia mfumo wa kisasa wa sauti na mambo mengine.
Dk Kashillilah akiwa amefuatana na Katibu Msaidizi wa Baraza la Wawakilishi na maofisa wengine wa Bunge la Jamhuri, alisema ratiba ya mkutano wa Bunge Maalumu la Katiba inaonesha kuwa litazinduliwa rasmi Februari 26, ingawa kesho litaanza kwa mkutano wa maelekezo ya ukaaji na jiografia ya ukumbi.
Alisema ratiba imeanza jana kwa kusajili wajumbe hao, kazi ambayo inaendelea leo na kesho asubuhi kutafanyika mkutano huo wa maelekezo na saa 8 mchana, kutasomwa tangazo la kuitisha Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda na kuandaa na kupitisha Kanuni za Bunge hilo.
“Mwenyekiti wa muda atachaguliwa kwa utaratibu maalumu uliowekwa na Katibu wa Bunge la Muungano na wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao utaratibu tutatoa kesho (leo). Mwenyekiti wa Muda atasimamia kuchaguliwa kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Dk Kashillilah.
Alisema Mwenyekiti wa Muda pia atasimamia kuandaliwa kwa Kanuni, na baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, ndipo atateuliwa Katibu na Naibu Katibu wa Bunge hilo kwa mujibu wa sheria kwani yeye na mwenzake wa Zanzibar, kwa sasa wanasimamia tu mchakato huo.
Alisema kabla ya Mwenyekiti na Makamu wa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba kuanza kazi zao, kwanza watasubiri Rais kuwaapisha Katibu na Naibu Katibu, na ndipo Katibu wa Bunge hilo, atakuja kumwapisha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti; na Mwenyekiti kuwaapisha wajumbe wake.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Jumatano na Alhamisi zitatumika kwa kikao cha kazi cha kuandaa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu, wakati Ijumaa itakuwa siku ya kupitisha Azimio la kuridhia Kanuni za Bunge Maalumu, uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na kiapo cha Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalumu (ingawa hiyo siyo shughuli ya Bunge Maalumu).
Dk Kashillilah alisema Jumamosi, itakuwa ni kiapo cha Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na kufuatiwa na kiapo cha wajumbe wa Bunge Maalumu ambacho kitaendelea hadi Jumapili.
Aidha, Jumatatu pia kutakuwa na kiapo cha wajumbe saa 4 asubuhi na kuunda Kamati za Bunge Maalumu, kabla ya ufunguzi rasmi wa Bunge utakaofanywa na Rais Jakaya Kikwete, saa 10 jioni.
Katibu huyo wa Bunge la Muungano alisema uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba kwenye Bunge Maalumu itakuwa ni Jumanne na Jumatano ya Februari 26, mjadala wa kupitisha Rasimu ya Katiba utaanza hadi Aprili 30, mwaka huu.
Kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Bunge Maalumu litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya Katiba inayopendekezwa na kutunga masharti ya Mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalumu litakavyoona inafaa.
Kupitisha Katiba Ili Katiba inayopendekezwa ipitishwe katika Bunge Maalumu la Katiba, itahitajika kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalumu kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, muda ambao Bunge Maalumu litajadili Rasimu ya Katiba hautazidi siku 70 kuanzia tarehe ambayo Bunge Maalumu lilipoitishwa, hivyo uhai wa Bunge hili unatarajiwa kukoma Aprili 30, mwaka huu, lakini unaweza kuongezwa kwa mashauriano kati ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu na Makamu wake kwa ridhaa ya Rais kwa kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia gharama za ukarabati wa jengo na miundombinu mingine, Dk Kashillilah alisema ni Sh bilioni 8.2, ambazo zote zimetoka katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/14 ambayo ilishapitishwa na Bunge ikiwamo posho za wajumbe ambazo ni Sh 300,000 kwa siku kwa mjumbe.
“Fedha zote hizo zilikuwapo katika Bajeti ya Serikali iliyopitishwa Juni mwaka jana, kwa hiyo siyo suala geni. Na zimetumika katika ukarabati wa jengo la ukumbi, vifaa vikiwamo viti 678 ambavyo gharama yake ni dola za Marekani milioni moja,” alifafanua Katibu wa Bunge.
Alisema katika posho, wajumbe watalipwa posho ya kawaida ya Serikali ya siku (haikutaja), lakini alisema kutawakuwa na kodi maalumu ambayo itahusisha posho ya kikao, usafiri, malipo kwa madereva na mengineyo, ambayo itakuwa ni Sh 220,000.
Hivyo posho ya kawaida itakuwa Sh 80,000 ukijumuisha na Sh 220,000 unapata Sh 300,000 watakazolipwa kwa siku.
Alisema Bunge Maalumu litajumuisha wajumbe 629 ambao ni wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 357, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW) 82 na wajumbe wa kuteuliwa kwa uwakilishi 201.
Aliongeza katika idadi hiyo, unapunguza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ambao pia ni wajumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sita, Mjumbe wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa uteuzi wa Rais wa Zanzibar, wabunge wawili waliofariki na nafasi mbili za uteuzi wa Rais zilizo wazi, unapata wajumbe 629, ambao zaidi ya 120 walikwisha jisajili hadi kufikia jana mchana.

Sunday, 16 February 2014

Kigwangala ataka muda wa Rais Madarakani Uongezwe.

hamisi
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Hamisi Kigwangalla amesema ili kuondoa mvutano kuhusu muundo wa Muungano ni lazima yafanyike mambo mawili, ambayo ni kuongeza muda wa Rais kuwa madarakani au kubadili Katiba katika maeneo yanayohusu Tume ya Uchaguzi (NEC) pekee.
Akizungumza jijini jana, Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega (CCM) alisema mambo hayo mawili hayawezi kukwepeka kwasababu hata kama Katiba Mpya itapatikana, bado itahitajika kufanya mabadiliko ya sheria mbalimbali, zoezi ambalo alidai litachukua takriban miaka miwili.
“Namwomba Rais Jakaya Kikwete aingilie kati. Atumie mamlaka yake kusitisha mchakato wa Katiba mpaka itakapoundwa Tume nyingine ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la muundo wa Muungano,” alisema na kuongeza;
hamisi
“Baada ya maoni hayo ipigwe kura maalumu kuhusu jambo hili ili Watanzania washiriki kikamilifu na upatikane uamuzi sahihi na unaokubalika na wengi. Si jambo la busara kujadili Rasimu ya Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu muundo wa Muungano.”
Alisema kuwa kitendo cha Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kupendekeza muundo wa Serikali tatu, utalivuruga Bunge la Katiba iwapo wataibuka wajumbe na kupinga muundo huo.
Alisema kuwa kama muundo wa Serikali tatu utapingwa, muundo wowote utakaopitishwa utasababisha kuwekwa vifungu vipya jambo ambalo litazidi kuleta mkanganyiko katika mchakato mzima wa Katiba.
“Ndiyo maana nikasema mchakato huu usitishwe kwa muda ili watu wote tukubaliane juu ya muundo wa muungano tunaoutaka. Wabunge wa Bunge la Katiba tukiukataa huu muundo wa Serikali tatu kipi kitatokea?”alihoji.
Dk Kigwangalla alisema Tume hiyo bado haijatoa majibu katika mambo kadhaa; njia ilizotumia kupendekeza Serikali tatu, kwa nini walipendekeza mfumo huo na nani atakuwa na mamlaka ya kuandika Katiba ya Tanganyika.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati tayari Rais Kikwete ameshateua wajumbe 201 wa Bunge hilo ambalo linaanza Februari 18 mjini Dodoma.

CHADEMA yatishia kususia bunge la Katiba…!!

mbowe
WAKATI keshokutwa Bunge Maalum la Katiba linaanza kukutana mjini Dodoma, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema huenda kikasusia Bunge Maalum la Katiba iwapo litaendeshwa kwa kufuata matakwa ya chama cha siasa na siyo ya wananchi.
 
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema hayo jana wakati akielezea maamuzi ya Kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika jana na kueleza kuwa chama hicho kinaenda katika Bunge hilo kikiwa na hadhari ya hilo.
 
Alisema wanaenda kwenye kikao hicho wakiwa na masikitiko kutokana na uteuzi wa wajumbe 201 wa bunge hilo waliotangazwa hivi karibuni kuwa karibu asilimia 75 hadi 80 ni wanaCCM.
  mbowe
Akijibu hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema “Tumewazoea, sio mara ya kwanza kususa waache wasuse najua nia yao tangu mwanzo ni Katiba isipatikane. Katiba mpya itapatikana hata wakisusa”.
 
Naye Mbowe alifafanua “Hatuendi katika bunge hilo kugoma lakini mambo yakienda visivyo kwa kufuata matakwa ya chama cha siasa na siyo mapendekezo ya rasimu ya pili ya Katiba hiyo ambayo ni ya wananchi tutalizira Bunge hilo,” alisema.
 
Alibainisha kuwa chama hicho hawatasita kurejea kwa wananchi wakati Bunge likiendelea au likiwa limeisha iwapo wingi wa wabunge wa chama tawala utaathiri Bunge hilo.
 
“Sasa wananchi watatuelewa dhamira yetu ya kutaka wajumbe hao wasiteuliwe na Rais kwani tulibishana sana lakini baadaye tulikubaliana jambo ambalo limeonesha kwa kuteuliwa makada wengi kwa manufaa ya chama tawala,” alisema Mbowe.
 
Alisema ingefaa makundi yenyewe yangeteua wawakilishi wao na siyo kupeleka kwa Rais hivyo Bunge hilo linaloanza keshokutwa wanaenda kwa tahadhari.
 
Vikao vya Bunge Maalum la Katiba linatarajia kuanza keshokutwa likihusisha wajumbe ambao ni wabunge wote wa Baraza la Wawakilishi ,Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na wajumbe 201 walioteuliwa na Rais Jakaya Kikwete akishirikiana na Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein.
 
Wajumbe hao 201 wameteuliwa kutoka makundi tofauti yakiwemo ya Taasisi zisizo za kiserikali, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Taasisi za dini, Taasisi za elimu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vinavyowakilisha wakulima, wafugaji, wavuvi na kundi la watu wenye malengo yanayofanana.
 
Bunge hilo litahusisha wajumbe takriban 650 wanaokwenda kuijadili rasimu ya pili ya Katiba na watatumia siku 70 na iwapo hazitatosha wataongezewa siku 20 ili kukamilisha mjadala huo. Kitakachofuata baada ya Bunge Maalum la Katiba ni wananchi kupiga kura ya maoni kupitisha Katiba hiyo mpya.
 
Katiba hiyo mpya itafuta Katiba ya sasa iliyodumu tangu Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961 na mabadiliko kadhaa yaliyofuatia baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
 
Alipoulizwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye amesema “tumewazoea, sio mara ya kwanza kususa waache wasuse najua nia yao tangu mwanzo ni Katiba isipatikane. Katiba mpya itapatikana hata wakisusa”.