Mwandishi vitabu Binyavanga Wainaina aliyetangaza majuzi kuwa anashiriki mapenzi ya jinsia moja
Mbunge
Irungu Kang'ata anaongoza juhudi za kundi lililoundwa majuzi la kupinga
wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya. Sheria zilizopo zasema ni hatia kwa
watu kujiingiza katika tabia za ushoga na adhabu yake ni kifungo cha
miaka 14 jela.
Kenya
huenda ikawa nchi inayofuata kwenye utata unaohusiana na haki za wapenzi
wa jinsia moja, huku wabunge wakipanga kuwasilisha mswada bungeni
kushinikiza serikali kufanya juhudi zaidi kutekeleza sheria zilizomo za
kupiga marufuku ushoga.
Nao
wanaharakati wa kutetea haki za wapenzi wa jinsia moja wanasema
shinikizo limeongezeka tangu nchi jirani ya Uganda kupitisha sheria
dhidi ya mashoga mwezi jana.
Irungu
Kang'ata, ambaye ni mbunge kwa mara ya kwanza anaongoza juhudi za kundi
lililoundwa majuzi la kupinga wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya.
Katika kampeni wazi kabisa mbunge huyo ameomba chama tawala kuelezea
serikali inachukua hatua gani kutekeleza sheria zilizopo dhidi ya
mashoga.
Sheria
zilizopo nchini Kenya zinasema ni hatia kwa watu kujiingiza katika tabia
za ushoga na adhabu yake ni kifungo cha miaka 14 jela. Hakuna aliyewahi
kushtakiwa nchini humo, lakini wanaharakati wanasema kuna kesi takriban
8 mahakamani ambazo hazijaamuliwa.
Kundi
hilo linalopinga wapenzi wa jinsia moja liliundwa majuzi wakati rais wa
nchi jirani ya Uganda Yoweri Museveni alipotia saini sheria dhidi ya
wapenzi wa jinsia moja mwezi Februari, licha ya shinikizo kutoka kwa
nchi za Magharibi asitie saini.Sasa ushoga huko Uganda ni kosa
linaloweza kuadhibiwa kwa kifungo cha maisha jela.
Mbunge
Kang'ata anasema anataka kuwasilisha mswada mpya utakaokuwa na adhabu
kali zaidi nchini Kenya ikiwa bunge litaamua kuwa sheria zilizopo hivi
sasa hazitoshi. Na anawashauri mashoga wajiepushe na matatizo haya kwa
'kufyata midomo'.
Lakini
kwa mkurugenzi wa kundi la kitaifa la tume ya haki za mashoga Kenya,
Eric Gitari anasema shinikizo hili dhidi ya wapenzi wa jinsia moja ni
njia moja ya kugubika matatizo ya kisiasa yaliyomo na ukiukwaji wa haki
za kibinafsi.
Gitari
ambaye ni wakili wa kutetea haki za binadamu, anapinga pendekezo kwamba
wapenzi wa jinsia moja wakae kimya, akisisitiza kuwa ni wanasiasa
wanaolieneza swala hili kwa umma. Kama mwanamume ambaye ni shoga anasema
mara nyingi anajihisi kama raia wa daraja la pili.
Naye
mwanaharakati wa kibinafsi Kenne Mwikya, anasema hisia nchini Kenya
zinaweka mazingira yafaayo kwa watu kama mbunge Irungu Kang'ata kuamua
kuwa wanapaswa kubuni sheria mpya dhidi ya wapenzi wa jinsia moja au
kutekeleza sheria zizilizopo.
0 comments:
Post a Comment