Kubishana sawa, lakini tuchunge kauli zetu!
Wote
sisi, kama binadamu huwa tunashikwa na hasira kutoka muda fulani hadi
mwingine, lakini kushikwa na hasira na kuziacha hasira hizo ziwaumize
wale tunaodai kuwa tunawapenda ni jambo tofauti sana.
Tunapojikuta
tunashindwa kuzuia kulipukwa na hasira dhidi ya wale tunaowapenda mara
kwa mara, inapasa tujue pia kwamba tunaujeruhi uhusiano wetu na baadae
tutauuwa kabisa.
Kuna
wakati kwa sababu mbalimbali, baadhi yetu huwa tunajikuta tukitaka tu
kuwakera wapenzi wetu kwa kuwapandishia kila wakati kwa milipuko ya
hasira. Ni kama vile, bila kulipukwa na hasira hizo, maisha yetu
yanakuwa yamepoteza maana.
Ni
vigumu sana wakati mwingine kwa watu hawa kuacha tabia yao hiyo, lakini
juhudi ya kujitoa ni muhimu sana. Ni muhimu sana kwa sababu, uhusiano
mwingi umevunjika kutokana na hasira hizi za kila wakati, ambazo wala
hazina msingi, bali zinatokana na mtu kujichukia mwenyewe.
Kutokana
na hasira hizi, mara nyingi wapenzi hujikuta wakilazimika kubishana
badala ya kujadili. Hawa watu wenye hasira hizi za hapa na pale, huwa
siyo wasikilizaji, bali ni watu wa kulaumu, kujitetea, na kutaka
kusikilizwa wao tu, kwa maana ya kushinda.
Katika
uhusiano wa aina hii, hakuna uwezekano wa ustawi, bali uwezekano ni
uhusiano kufa. Kwani ni mara chache ambapo huyu mpenzi mwenye hasira za
mlipuko atakuwa tayari kusikiliza na kuelewa.
Jambo
ambalo wapenzi wanapaswa kulifanya,. Bila kujali kama wana hasira sana
au hasira nyingi, ni kujitahidi kuweka nguvu kwenye jambo wanalojadili.
Watu wenye hasira za ziada, huwa hawana uwezo wa kuzingatia kile
kinachojadiliwa.
Huwa
na ugumu huo kwa sababu hasira za ziada huwasukuma kusema chochote
ambacho kitawafanya washinde, ikiwemo kusingizia na kusema uongo. Lakini
huwa wanabebwa na wimbi la hasira kiasi kwamba hawana muda wa kupima
athari ya kile wanachosema.
Kuna
haja ya kujua kwamba, neno moja tu la hasira, linatosha kuvunja
uhusiano au ndoa. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa mtu mwenye hasira za
mlipuko kujifunza kuzingatia jambo ambalo, yeye na mpenzi wake
wanalijadili. Anapotoka nje ya mada, ni lazima ataropoka.
Kuna
wanandoa wanabishana kuhusu shule ya mtoto kwa mfano, mwanandoa
mwingine hana haja ya kusema, ‘unabisha kwa sababu hukusoma, ndilo
tatizo la kuoa wanawake wasiosoma.’ Hapa ni kutoka nje ya mada kwa
hasira za mlipuko.
Kumbuka
pia kwamba, wanandoa au wapenzi ambao wanapobishana hawatoki nje ya
kile wanachobishania na pia wanatumia nguvu ya hoja badala ya mihemko,
huwa wanaelewana katika mambo mengi sana, huwa wanatatua migogoro mingi
kwa amani na kuaminiana zaidi.
Kuna
wakati kwa sababu ya hasira za mlipuko, mpenzi anaweza kutafuta kwa
makusudi jambo ambalo litamuudhi mpenzi wake. Anaweza kumwambia,
‘sibishani na mwanamke mnene kama nguruwe.’ Au mwanamke akamwambia
mpenzi au mumewe, ‘mbele ya wanaume nawe unajiita mwanaume.’
Kila
mmoja wetu anajua ni maneno gani akisema yatamkera mwenzake. Nasema
kila mpenzi anajua eneo nyeti la mpenzi wake, ambalo akiligusa anakuwa
amemuuwa kisaikolojia. Kujua huku eneo hilo hakupaswi kutumiwa vibaya na
wapenzi.
Kwenye
uhusiano kuna kanuni ya, ‘usimtendee mwenzio yale ambayo hupendi
kutendewa.’Wapenzi wanapoweza kila mmoja kufuata kanuni hii, uhusiano
huwa mzuri sana.
Kuna
wakati mpenzi anaweza kudhani kwamba wakati wa kubishana ndio wakati
mzuri kwake ‘kumpasha’ mpenzi wake, ndiyo wakati mzuri wa kumuumiza
kihisia. Hili ni kosa la karne kwa sababu wakati huu, ndio ambao
mwanandoa au mpenzi anapopaswa kujilinda na kauli zake kuliko waati
mwingine.
Maneno
ndio silaha kwenye kubishana kumbuka. Kwa hiyo yanatumika vizuri au
vibaya ni jambo la msingi sana. Maneno huumiza na kuvunja mifupa kuliko
vyuma, anavyoweza kupigwa navyo mtu.
Mtu
anapojifunza kubishana bila kutumia maneno ya kuumiza au kutoka nje ya
mada inayojadiliwa, hujenga kujiamini, kwani mara nyingie hasira za
ziada ni matokeo ya kutojiamini.
Inaonekana kuna aina ya maradhi ya kisaikolojia, ambapo mtu hujikuta hawezi kuishi maisha ya amani na mpenzi.
Akihisi
amani ni kubwa, hutafuta njia ya kuiondoa ili ajisikie vizuri. Kwa
hiyo, atazua jambo ambalo litazua ubishi ambao utamfanya aropoke.